Tuesday, January 8, 2013

Wanasiasa wawasha moto Tume ya Katiba

Wanasiasa wawasha moto Tume ya Katiba

Ndg. Andrew Chenge akiwasilisha maoni ya chama chake kuhusu Katiba Mpya katika mkutano na Tume ya Mabadiliko ya Katiba 


Posted  Jumatatu,Januari7  2013  saa 20:55 PM
Kwa ufupi
CHADEMA WATAKA UMRI WA URAIS USHUSHWE, CUF WALIA NA MUUNGANO WA MKATABA, CCM WABEBA LA MGOMBEA BINAFSI

TUME ya Mabadiliko ya Katiba, jana ilianza kukusanya maoni ya vyama vya siasa katika mchakato wa Katiba Mpya, huku baadhi ya vyama hivyo vikitoa mapendekezo mbalimbali kuhusu suala la urais.
Vyama vilivyozungumzia urais katika mkutano huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam ni CCM, CUF na Chadema.

Taarifa za vyama hivyo zilipatikana baada ya wawakilishi wao kuwasilisha maoni kwenye tume hiyo katika mkutano wa ndani ambao waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia.

Wakati CCM ikitaka Katiba ijayo iruhusu mgombea binafsi, Chadema imependekeza Mtanzania yeyote mwenye umri wa kuanzia miaka 18 aruhusiwe kupiga kura na kugombea nafasi yeyote ya uongozi nchini. CUF imependekeza Muungano wa Mkataba.

Mwanasheria wa Chadema ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alisema chama hicho cha upinzani, kimependekeza Katiba Mpya imtambue mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 18 kuwa ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa kushika nafasi yoyote ya uongozi nchini.

“Haingii akilini kwa mtu mwenye umri wa miaka 18 anakubalika kupiga kura na kumchagua kiongozi anayemtaka, lakini yeye mwenyewe hakubaliki kugombea nafasi yoyote ya uongozi ikiwamo urais, ubunge na udiwani,” alisema Lissu.

Alihoji “Kama Katiba ya sasa inamtambua mtu mzima kuwa ni yule anayeanzia umri wa miaka 18, kwa nini linapokuja suala la kuchaguliwa kwa ngazi zote ananyimwa haki hiyo hata kama ana vigezo vingine?”
Pia Lissu alisema kuwa Katiba Mpya haina budi kuanzisha utawala wa majimbo yasiyozidi kumi ili kuleta uwiano katika matumizi ya rasilimali kwenye maeneo yote ya nchi.

Aliyataja majimbo hayo kuwa ni Jimbo la Nyanza Magharibi ambalo litajumuisha mikoa ya Kagera, Geita na Shinyanga; Nyanza Mashariki mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu, Ziwa Tanganyika kwa mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa na Jimbo la Kati litakalojumuisha mikoa ya Dodoma, Tabora, Singida na Iringa.

Mengine na mikoa yake kwenye mabano ni Jimbo la Kaskazini ( Arusha, Manyara na Kilimanjaro), Pwani ya Kaskazini (Tanga, sehemu za Pwani na sehemu za Morogoro), Jimbo la Dar es Salaam, Jimbo la Pwani Kusini (Mtwara, Lindi, Wilaya za Mafia, Rufiji na Ulanga) na Kanda ya Nyanda za Juu (Njombe, Mbeya na Ruvuma).

Mwakilishi wa CCM, Andrew Chenge alipendekeza kuwapo kwa mgombea binafsi katika nafasi zote ili kutoa fursa ya wananchi wasio wanachama wa chama chochote cha siasa kupata nafasi ya uongozi.

Alisema, kitakachofanyika ni kitengeneza mazingira mazuri ambayo yatawezesha mgombea huyo kupatikana bila ya kuwapo kwa itikadi za udini au ukabila.

“Mapendekezo ya chama chetu ni kuwapo kwa mgombea binafsi ili kushiriki kwenye nafasi zote za uongozi. Hii itasaidia kuondoa ubaguzi au kuleta udini, jambo ambalo linaweza kutoa fursa kwa wananchi wasio na udini wala chama kushiriki kwenye nafasi ya uongozi,”alisema Chenge.

CUF Serikali tatu
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema kuwa, chama hicho, kimependekeza kuwa na mkataba katika masuala mbalimbali yanayohusu Muungano.

No comments:

Post a Comment